Mtalam III Mtalam III Author
Title: Daz Baba awe mfano kwa wasanii wengine wa Bongo flava
Author: Mtalam III
Rating 5 of 5 Des:
Unalikumbuka vizuri lile kundi la wale vijana wa Temeke, Daz Nundaz? Nini TMK Family, hawa madogo walikuwa balaa. Kamanda ndiyo ulikuwa wimb...
Unalikumbuka vizuri lile kundi la wale vijana wa Temeke, Daz Nundaz? Nini TMK Family, hawa madogo walikuwa balaa. Kamanda ndiyo ulikuwa wimbo wao maarufu zaidi na uliotikisa anga lote la Bongo Fleva.
Kulikuwa na vichwa vitano vilivyotengeneza crew hii. Ferooz, Daz Baba au Daz Mwalimu, Sajo, Larumba na Critic. Kama ambavyo imetokea kwa makundi mengi, Daz Nundaz sasa imebakia historia.

Mmoja wa nyota waliokuwa gumzo kundini humo ni Daz Baba, yule dogo mwenye mwili mdogo, akisokota nywele zake katika staili ya rasta, aliyependa kutembea kwa mikogo.

Daz alijua kuifanya kazi yake vizuri. Licha ya kufanya kazi na kundi, lakini jamaa aliweza pia kutengeneza nyimbo zake kadhaa binafsi ambazo zilifanya vizuri, kitu kilichosaidia sana kumpatia shoo nyingi katika maonesho mbalimbali.

Kuna kibao kama Umbo Namba Nane aliofanya mkongwe wa Hip Hop, Fid Q. Ni kibao kilichokamata sana na kutamba katika chati za redio mbalimbali nchini.

Aliwahi pia ‘kusumbua’ na nyimbo zake nyingine kama Wife aliomshirikisha marehemu Ngwair, Nipe Tano aliowapa shavu Daz Nundaz, Elimu Dunia aliokwenda sambamba na Afande Sele.

Umaarufu ulikuwa mkubwa kwa Daz Baba na kama ilivyo kwa vijana wengi wanaojihusisha na muziki huo, akawa kipusa. Apite wapi asijulikane. Uzuri wa mastaa wetu, wanajijua, wanajua wanatazamwa wanapopita, lakini hawataki kujua pia kwamba vitendo vyao vinaonekana.

Bangi katika Bongo Fleva siyo jambo la ajabu. Wengi wanavuta, lakini taratibu habari zikaanza kuzagaa mitaani kuwa Daz Baba anatumia dawa za kulevya. Alijitahidi kukataa, lakini macho ya watu yalimuona.

Tatizo moja la watu wa Bongo Fleva, wanaamini utumiaji wa madawa ya kulevya ni ujanja, kwamba ukitumia ndiyo utaonekana mtoto wa mjini, asiye mshamba. Ni kwa vile tu hawajui hatima yao ya baadaye, lakini ukweli ni kwamba hawa ambao wao wanawaona washamba, ndiyo wajanja halisi.

Daz Baba alianza kupoteza mwelekeo taratibu, akionekana vijiweni kwa muda mwingi, hatimaye akafanana kabisa na wale mateja tunaowaona katika stendi za madaladala wakipiga debe.

Miezi michache iliyopita, alionekana mjini Morogoro akiwa kama mtu aliyechanganyikiwa kabisa. Ni jambo la kusikitisha sana kugundua kwamba mtu ambaye jamii ilimtegemea kwa burudani, mafunzo na mfano, sasa amegeuka kuwa kituko.

Lakini kama nilivyosema mwanzo, hii inatokana na mawazo duni ya kutojitambua kwa wengi wa wasanii wetu, fedha na umaarufu wanaoutafuta kwa shida kubwa, huwaletea usumbufu katika maisha yao ya kila siku.

Wasanii wetu wanaposikia Chris Brown, Snoop Dog, Jay Z, Whitney Houston au 50 Cent  wanatumia madawa ya kulevya, nao hukimbilia kujitumbukiza bila kujua kwamba wana tofauti kubwa na mastaa hao wa Marekani kwa kila kitu.

Wenzao wana mameneja wanaojua kazi zao, wana pesa nzuri na hata vipimo vya utumiaji wa dawa hizo. Hawajidungi tu ovyo kama wanavyofanya wa kwetu, ndiyo maana unawasikia wakiendelea kuwepo licha ya habari zao kuanza kusikika miaka mingi.

Nichukue tena nafasi hii kuwashauri wasanii wetu wanaoubwia unga na kufanya mambo mengine yasiyostahili mbele ya jamii. Wao wanapaswa kuwa vioo vya wanaowazunguka kujitazama.

Wanayo nafasi kubwa sana ya kusaidia juhudi za serikali katika kutatua tatizo la ajira. Wanapata fedha, wawekeze katika miradi mbalimbali ili wenzao walio vijiweni wapate ajira, kitu ambacho kitasaidia pia kupunguza uhalifu.

Source: Global Publishers


Matangazo | Click them for more details:

• Tablet aina ya ‘Swag Tab - Expert 102’ Inauzwa kwa bei nafuu
• Simu aina ya ‘Nokia N9’ Inauzwa kwa bei nafuu

Like Keezywear on Facebook!

Author

Advertisement

 
Top